Kocha Mkuu wa Mwadui FC, Amri Said amepanga kuboresha safi yake ushambuliaji kwa kupendekeza usajili wa mshambuliaji wa Young Africans Ditram Nchimbi, ambaye amekosa nafasi ya kucheza mara kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Cedric Kaze.
Amri Said ambeye amechukua mikoba ya kocha Khalid Adam aliefutwa kazi mwishoni mwa mwaka jana(2020), amesema anaamini usajili wa mshambuliaji huyo utaongeza chache kwenye kikosi cha Mwadui FC, ambacho msimu huu kina changamoto ya kupata matokeo.
Kocha huyo mzawa amesema mbali na usajili wa mshambuliaji huyo ambaye huenda akatua Mwadui Complex kwa mkopo, pia amepanga kufanya mabadiliko katika idara nyingine kwenye kikosi chake, ili kuwa na mwanzo mzuri kwenye mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Mzunguko wa pili tutafanya kazi kubwa kwa kuhakikisha kwamba tunapata matokeo mazuri ndani ya uwanja na ni jambo la msingi kwetu kuweza kupata matokeo.”
“Kikubwa wachezaji ambao tutawaongeza kwenye dirisha dogo ninaamini kwamba watakuwa na msaada kwetu hivyo mipango ikakamilika kila kitu kitawekwa wazi.”
Mwadui FC kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ipo nafasi ya 16 ikiwa na alama 15 baada ya kucheza michezo 18.
Wakati huo huo taarifa zinasema kuwa, Uongozi wa Mwadui FC umetuma barua za maombi ndani ya Young Africans ukihitaji kumpata Nchimbi, na kama mambo yatakuwa magumu basi wameomba wapewe nyota Wazir Junior akaokoe jahazi.
Nchimbi amewahi kucheza ndani ya Mwadui FC kwa mkopo akitokea Azam FC kabla ya kuibukia Polisi Tanzania na badae kusajiliwa Young Africans.