Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki katika Mkutano wa 111 wa Shirika la Kazi Duniani (ILC 111) unaofanyika jijini Geneva, Uswisi katika Makao Makuu ya Shirika hilo.
Akizungumza katika Mkutano huo, Prof. Ndalichako ameeleza baadhi ya masuala ambayo Tanzania imeyatekeleza katika kukuza usawa mahali pa Kazi ikiwemo marekebisho ya Sheria katika Sekta ya Hifadhi ya Jamii, ili kuongeza wigo wa Hifadhi ya Jamii katika Sekta isiyo rasmi.
Mengine ni kutangazwa kwa kima cha chini cha mshahara na kuendelea na mapitio ya sheria za kazi ili kuimarisha utekelezaji wa Kanuni za Msingi na Haki za Kazi (Principles and Rights at Work) na kutunga Kanuni Sita zinazohusu masuala ya Afya na Usalama pa Kazi na kwamba Serikali inaendelea kugharimia Programu za Mafunzo ya Ukuzaji Ujuzi kwa Vijana.
Aidha, amewasilisha maoni na mchango wa Tanzania katika Ripoti ya Mkurugenzi Mkuu wa ILO Gilbert Houngbo, ambayo imesisitiza nchi wanachama kukuza na kudumisha Usawa Kitaifa na Kimataifa hasa kwa makundi ya wafanyakazi ambayo yapo katika hatari kubwa ya kuathirika na aina mbalimbali za unyanyasaji.
Waziri Ndalichako pia amesisitiza utayari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza ushirikiano na ILO pamoja na wadau wengine katika kutekeleza mikataba mbalimbali ya Shirika hilo.