Mkurugenzi wa ufundi wa Ndanda FC Hamim Mawazo, jana alianza zoezi la kusaka wachezaji ambao watakiongezea nguvu kikosi cha klabu hiyo ya mkoani Mtwara.
Katibu mkuu wa Ndanda FC Suleyman Kachele, amesema zoezi hilo limeanza vizuri, na wana matumaini makubwa na mkurugenzi wao wa ufundi, kwa ajili ya kufanikisha upatikanaji wa wachezaji ambao watakuwa na jukumu la kuunda kikosi kipya.
Amesema jukumu lao kwa sasa ni kuunda kikosi kitakachokua na mchanganyiko wa wachezaji wazoefu na vijana, huku akiangalia namna ya kuwa na matumizi madogo ya kifedha ya kukiendesha kikosi hicho.
“Vijana wamejitokeza kwa wingi, idadi yao ni kama 50 hivi, tunaamini Hamim Mawazo atafanikisha zoezi hili na kuwapata wachezaji ambao wana sifa ya kucheza soka la kupambana.
“Kwa sasa zoezi hili linafanyika kwa wahusika kujitegemea kwa kila kitu, lakini tukifanikiwa kuwapata wachezaji watakaopitishwa na mkurugenzi wa ufundi, wataingia katika mamlaka ya kuhudumiwa na klabu.” Amesema Kachele.
Katika hatua nyingine Suleyman Kachele amesema uongozi wa Ndanda FC kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa Mtwara, unaendelea kusaka wadhamini na wafadhilia mbao watasaidia kufikia lengo la bejeti waliyojiwekea, ili kuwezesha ushiriki wao mzuri kwenye ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu ujao.
“Tunaendelea kuhangaika kwa kushirikiana na serikali ya mkoa, tunaamini mpango kazi uliopitishwa kwa pamoja unaweza kutusaidia ili kufikia lengo la kupata fedha za kukiendesha kikosi chetu.
“Bajeti tuliyoipitisha kwa ajili ya kila kitu mpaka mwishoni mwa msimu huu, ni kama bilioni 1.1, tunafahamu ni fedha nyingi sana na huenda ikawa ngumu kupatikana zote kwa mara moja.
“Kwa kuanzia tunaangalia uwezekano wa kupata hata robo yake ili tukamilishe usajili, halafu jitihada nyingine za kutafuta nusu na robo zitakua zikiendelea chini ya ushirikiano kati yetu na serikali ya mkoa wa Mtwara.”
Ndanda FC imekua katika matatizo ya fedha kwa kipindi kirefu na karibu misimu yote waliyoshiriki ligi kuu wamekua wakishindwa kujizatiti katika michezo yao kwa kutowalipa wachezaji vizuri, hali ambayo huhatarisha uimara wa kikosi na kunusurika kushuka daraja.