Mbunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Halima Mdee amesema kuwa ndani ya vyama vya upinzani kuna matatizo, ndio maana vimekuwa vikiungana kipindi ambacho muda unakuwa umeenda na matokeo yake kupelekea kufanya maamuzi ya haraka.
Amesema kuwa hali hiyo inachangiwa na mapungufu ndani ya vyama hivyo, na kuzidiwa na nguvu kubwa kutoka nje.
“Changamoto ambayo imekuwepo miaka yote tangu mfumo wa vyama vingi uanze ni kwamba kila chama kimekuwa kikifanya kazi peke yake na tumekuwa tukiungana kwa kuchelewa, tukiwa tunaelekea uchaguzi mkuu ndio tumekuwa tunaungana na kukubaliana mambo kadhaa kwa haraka”, amesema Mdee.
Aidha, ameongeza kuwa kitu ambacho wanajaribu kukitafuta hivi sasa ni kutengeneza uongozi madhubuti, ili kudhibiti nguvu za nje na kujenga imani miongoni mwao.
Hata hivyo, vyama vya Upinzani nchini vimeazimia kuanza kufanya mikutano ya hadhara kuanzia mwaka 2019 kwa kile walichodai kuwa ni haki yao kisheria na kikatiba, hali ambayo inaonekana kuwa tofauti na msimamo wa serikali kuhusu suala hilo.