Kocha Mkuu wa Klabu ya Azam FC, Etienne Ndayiragije amewazungumzia wababe wa Simba katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, TP Mazembe kuelekea mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kagame inayoendelea nchini Rwanda.
Amesema kuwa awali hawakujipanga dhidi yao lakini baada ya ratiba kubadilika jana, ambapo hivi sasa watavaana na mabingwa hao mara tano wa Klabu Bingwa Afrika, akiwapa onyo kuwa Azam FC imejipanga kutetea ubingwa.
“Mabadiliko ya mchezo kwetu hayakutusumbua, tulikuwa tayari kuvaana na yeyote kwa sababu timu zote tumeziona kwahiyo tuko tayari kushindana nao. Nina wachezaji ambao wamechanganyika na vijana wadogo, kwa pamoja wataleta kitu katika michuano”, amesema Ndayiragije.
TP Mazembe na Azam FC zitacheza mchezo wa robo fainali ya kombe la Kagame kesho, Julai 16, ukifuatiwa na mchezo wa KCCA na Rayon Sports, APR FC na AS Maniema, huku mchezo wa mwisho ukiwa kati ya Gor Mahia na Green Eagles.