Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Etienne Ndayiragije ameendelea kumchunia kipa bora namba moja wa Simba SC, Aishi Salum Manula baada ya kumtenga katika kikosi cha awali cha wachezaji 27 kuelekea mechi na Equatorial Guinea Ijumaa ijayo.
Taifa Stars watakuwa wenyeji wa Equatorial Guinea katika mchezo wa Kundi J kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2021) nchini Cameroon Ijumaa ya Novemba 15 kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Kocha Ndayiragijje raia wa Burundi, kwa mara ya kwanza baada ya kuthibitishwa kuwa kocha Mkuu rasmi wa timu hiyo kufuatia kukaimu tangu Julai ametaja kikosi, ambacho pia kitatumika katika mchezo wa pili wa kufuzu AFCON dhidi ya Libya Jumanne ya Novemba 19.
Kikosi alichotaja Ndayiragijje kinaundwa na makipa; Juma Kaseja (KMC), Metacha Mnata (Yanga SC) na David Kisu (Gor Mahia).
Mabeki; Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Hassan Kessy (Nkana FC/Zambia), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba SC), Gardiel Michael (Simba SC), Erasto Nyoni (Simba SC), Bakari Nondo (Coastal Union), Kelvin Yondan (Yanga SC) na Dickson Job (Mtibwa Sugar).
Viungo; Jonas Mkude (Simba SC), Abdulaziz Makame (Yanga SC), Simon Msuva (Difaa El Jadida/Morocco), Eliuter Mpepo (Buildcon/Zambia), Iddi Suleiman (Azam FC), Salum Abubakar (Azam FC), Muzamil Yassin (Simba SC), Frank Domayo (Azam FC), Farid Mussa (Tenerife/Hispania), Hassan Dilunga (Simba SC).
Washambuliaji; Kelvin John (huru), Ayoub Lyanga (Coastal Union), Ditram Nchimbi (Polisi Tanzania), Shaaban Iddi (Azam FC), Miraj Athumani ‘Madenge’ (Simba SC) na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji).