Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) leo alfajiri kiliwasili jijini Dar es salaam, kikitokea nchini Tunisia kilipokua na mtihani wa kuikabili timu ya taifa ya Libya kwenye mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2021).
Stars ilipoteza mchezo huo uliochezwa juzi Jumanne mjini Monastiri, Tunisia kwa kufungwa mabao mawili kwa moja, hali ambayo imelifanya kundi J kuwa na timu mbili zenye alama tatu, huku Tunisia wakiongoza kwa kufikisha alama sita, na Equatorial Guinea wakiburuza mkia kwa kuambulia patupu, baada ya kushuka dimbani mara mbili.
Baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa julias Nyerere, kocha mkuu wa Taifa Stars Etinne Ndayiragije alizungumza na waandishi wa habari na kusema hashangazwi na wadau wanatofautiana na plani zake kwenye mchezo wao dhidi ya Libya waliopoteza kwa mabao 2-1, akijibu bado hana presha na kwamba mipango yake ilikuwa sahihi sema tu bahati iliwaangusha Tunisia
Amefafanua kwamba kila kocha ana mitazamo yake hivyo asingeweza kukichezesha kikosi chake kwa plani za Libya.
“Stars ni Stars na Libya ni Libya, ninachojua wachezaji wangu wanaendelea kupata uzoefu hivyo ninawatarajia watafanya makubwa kwenye michuano ya CHAN, Chalenji na kufuzu Kombe la Dunia,” amesema.
Ndayiragije amesema matokeo yanapokuja tofauti na matarajio ya mashabiki anaamini kunakuwa na changamoto za aina tofauti, jambo kubwa analotarajia kulifanya nikukaa chini na wachezaji kujua waanzie wapi.
“Tutapata muda mwingi wa kukaa pamoja na wachezaji ili kufanya maboresho kwa mapungufu yaliojitokeza ili kujiweka sawa kwa michuano ambayo ipo mbele yetu,”
“Watanzania waendelee kuiunga mkono timu yao, matokeo ni kati ya changamoto zilizopo kwenye soka yasifanye wakate tamaa bali nikuendelea kupambana kufikia ndoto zetu,”amesema.
Kwa matokeo ya juzi imeifanya Stars isalie na alama tatu ilizopata kwa kuichapa Guinea ya Ikweta mabao 2-1 nyumbani na sasa inasubiri majaliwa yake kwenye michezo ijayo mwakani watakapovaana na Tunisia ugenini na nyumbani.
Baada ya hapo itaifuata Guinea kurudiana nao na kumaliza michezo ya kuwania kufuzu mwezi Novemba dhidi ya Libya ili kujua kama itaenda AFCON 2021.