Baada ya shirikisho la soka barani Afrika CAF kuanika hadharani makundi ya michuano ya mataifa bingwa barani Afrika (CHAN), kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania *Taifa Stars* Ettiene Ndayiragije amesema kikosi chake kitakua na mabadiliko makubwa.
CAF walipanga makundi ya michuano ya CHAN juzi jumatatu jijini Cairo, Misri, na Tanzania iliangukia kundi D lenye timu za Namibia, Zambia na Guinea.
Kocha ndayiragije amesema amekua katika harakati za kufuatilia wachezaji kupitia michezo ya ligi kuu ya soka Tanzania bara inayoendelea hivi sasa, na ameona baadhi ya wachezaji ambao huenda akawaita kwenye kikosi kitakachoelekea Cameroon kushiriki michuano ya CHAN.
“Nimekua ninazunguuka kila eneo linalochezwa michezo ya ligi kuu ili kuona kina nani naweza kuwaita kwenye kikosi changu, nitahakikisha ninafanikisha zoezi hili, ili kufanikisha azma ya kuwa na wachezaji watakaokidhi vigezo vya kwenda kupambana.”
“Wachezaji tuliokua nao katika safari ya kufuzu fainali za CHAN, nao wanapaswa kujituma zaidi, kwa sababu nimeona kutakua na changamoto ya kuhakikisha wanabaki kwenye kikosi changu cha mwisho kitakachoelekea Cameroon. ” amesema Ndayiragije.
Hata hivyo kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema, atakiandaa vyema kikosi cha Taifa Stars, ili kuleta upinzani dhidi ya timu za kundi D, na kupata ushindi utakaowavusha hatua ya makundi.
“Bado hatujachelewa timu inaweza kuingia kambini hata wiki mbili tu ikafanya vizuri, kikubwa ni wachezaji wenyewe kuwa tayari na ninaamini Stars itafanya vizuri kwa sababu tulifuzu kwa uwezo wetu na tutajiandaa” amesema Kocha huyo.
Michuano ya CHAN imepangwa kuanza Aprili 4 hadi 25 mwaka huu nchini Cameroon.
Taifa Stars itaanza kampeni za kuwania taji la michuano hiyo mjini Limbe kwa kucheza dhidi ya Zambia, kisha itashuka dimbani kupapatuana na Namibia na itamaliza michezo ya hatua ya makundi dhidi ya Guinea.