Ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia, Boeing 737 iliyokuwa ikisafiri kutoka jijini Addis Ababa kuelekea Nairobi nchini Kenya imeanguka leo, muda mfupi baada ya kuruka ikiwa na watu 157.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika hilo la ndege, ndege hiyo yenye namba ET 302, ilipoteza mawasiliano ikiwa katika anga la jiji la Addis Ababa baada ya kuanza safari yake leo majira ya saa mbili asubuhi kwa saa za ukanda wa eneo hilo ikitokea katika Uwanja wa Kimataifa wa Bole.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa ndege hiyo ilianguka karibu na eneo la Bishoftu, Kusini Mashariki mwa Addis Ababa.
“Hadi sasa zoezi la utafutaji na uokoaji linaendelea na hatujapata taarifa zozote zilizothibitishwa kuhusu watu walionusurika au hata majeruhi,” imeeleza taarifa ya Ethiopian Airlines.
“Timu ya wafanyakazi wetu itatumwa kwenye eneo la ajali kwa ajili ya kutoa msaada wowote kadiri wawezavyo,” imeongeza.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ametumia mtandao wa Twitter kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa watu wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo.