Jumla ya watu 13 wakiwemo watoto 3 wamefariki baada ya ndege ya kivita ya Urusi kuanguka kwenye jumba la makazi ya raia katika mji wa kusini ya Yeysk, muda mfupi tu baada ya kupaa angani.
Katika tukio hilo, watu wengine sita hawajulikani walipo huku 19 wakijeruhiwa na inaarifiwa kuwa Yeysk imetenganishwa na eneo linalokaliwa na Urusi la kusini mwa Ukraine na Bahari ya Azov.
Jengo hilo la ghorofa tisa, limeonekana likiteketea kwa moto mkubwa, huku maafisa wakibaini kuwa kwa sasa moto huo umedhibitiwa ingawa shughuli za uopkoaji bado zinaendelea.
Hata hivyo, kamati ya Uchunguzi ya Urusi, ambayo inashughulikia masuala ya uhalifu imesema imeanzisha kesi ya jinai na kuwatuma wachunguzi kwenye eneo la tukio ili kubaini chanzo na kuchukua hatua.