Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeruhusu ndege zinazobeba watalii kuwasili visiwani humo, baada ya mambukizi ya virusi vya corona kupungua.
Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mahmood Thabit Kombo amesema kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa virusi vya corona si tishio kubwa katika sekta ya utalii.
Waziri wa Afya Zanzibar, amesema hadi sasa kuna wagonjwa 10 waliolazwa katika vituo vinavyotoa huduma za wagonjwa wa Covid -19 na Pemba kukiwa na mgonjwa mmoja.
Amesema baadhi ya vituo vilivyokuwa vikitoa huduma za wagonjwa tayari vimefungwa baada ya kukosa wagonjwa wa aina hiyo.
Hata hivyo Waziri Kombo amesema kuwa pamoja na serikali kuruhusu shughuli za utalii kuendelea, ni vyema shughuli hizo zikaendelea huku tahadhari dhidi ya corona ikiendelea kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na watalii kupimwa pindi wanapoingia visiwani humo.