SIMBA wamemtoa mkopo wa mwaka mmoja rafiki yangu Said Ndemla.

Wamempeleka Mtibwa Sugar na jana walimtambulisha kwenye page zao.

Kuna mengi ya kuyaandika hapa juu ya Ndemla, lakini leo tuyaache.

Kiufupi sana, nyuma ya usajili huu, mpira uko kwenye Mahakama ya Ndemla.

Uamuzi ni wake kujipa hukumu ya kushindwa au kushinda. Ni yeye.

Mastaa wengi wa timu kubwa walipojiunga na timu za daraja la Mtibwa Sugar maisha yaliwashinda.

Mtibwa Sugar hamsafiri na Ndege umbali mrefu, hampati bonus nzuri. Mishahara yenu sio minono kama mishahara ya timu kubwa.
Mbaya zaidi unakaa mbali na mjini.

Maisha haya yamewashinda mastaa wetu wengi.

Mastaa wachache ndiyo waliyaweza na baadae wakarudi kibabe mjini.

Inahitaji moyo kuyaishi maisha ambayo hukuwahi kuwaza kuyaishi.

Nawaelewa wachezaji waliokuwa mastaa wakubwa wa timu za Kariakoo kisha baadae wakaenda timu za mikoani.

Wanaishi maisha tofauti. Wanakutana na vitu vingi vigeni.

Mtafuteni Kelvin Yondani awahadithie maisha yake ya sasa pale Polisi Tanzania.

Sitamani rafiki yangu Ndemla auingie mkumbo wa kupaona Morogoro kama sehemu mbaya kufanyia kazi.

Aende Mtibwa Sugar akaonyeshe yeye ni kiungo wa namna gani. Wakubwa watamrudisha mjini kwa gharama kubwa. Hassan Dilunga ni moja ya mifano hai.

Dilunga alianza maisha yake pale Ruvu Shooting, baadae akaenda Yanga, maisha yalipomshinda akaanza kuzurura timu za mikoani.

Akaibukia Mtibwa Sugar na kufanya vyema Simba wakamuona. Wakamrudisha mjini.

Unamkumbuka fundi wa mpira Mohamed Ibrahim ‘MO’? Tangu aondoke Simba hajarudi tena kuwa MO yule. Maisha ya Namungo fc yalimshinda, maisha ya Kagera Sugar yakamshinda. Nimesikia mahala hivi sasa hana timu na msimu ujao atakuwa mtazamaji wa ligi.

Ndemla hajawahi kucheza timu nyingine zaidi ya Simba katika maisha yake ya mpira. Amelelewa Simba, amekuzwa Simba, mechi yake ya kwanza katika ligi alikuwa na jezi za Simba.

Ndemla alivyo, anahitaji utulivu wa akili, mwili ili arudi tena mjini.

La sivyo njia panda aliyosimama sasa anaweza kujikuta ameangekia upande wa kuwa Shetani.

Imeandaliwa na Abdul Mkeyenge.

Wahandisi wahimizwa kujisajili
Aweso atoa maagizo kwa wataalam wa maji safi