Kiungo Andrey Coutinho anaondoka nchini kurejea Brazil kwa kuwa mkataba wake na Yanga, umevunjwa rasmi.

Raia huyo wa Brazil naye amekiri kumalizana na Yanga na leo anatarajia kuondoka nchini kurejea kwao huku akisema: “Nitakumbuka sana Tanzania, acha nirudi nyumbani nikajipange.”

Coutinho aliingia katika mvutano wa siku nyingi na uongozi wa klabu hiyo ambapo wapo waliokuwa wakimhitaji na wapo waliokuwa wakimkataa huku akiwa siyo chaguo la kocha, Hans van Der Pluijm kufuatia kumuweka benchi.

Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, alifunguka  kuwa, tayari uongozi wa klabu hiyo umeshavunja mkataba wa miezi nane uliokuwa umebakia huku wakiwa katika mazungumzo na mchezaji mwingine kutoka nje ya nchi, kwa lengo la kuziba nafasi yake.

“Tangu awali nilieleza kuwa hatutasajili hadi atakapoondoka mtu, hivyo tayari tumeshaachana na Coutinho. Tunafanya mazungumzo na mchezaji kutoka nje ya nchi kuweza kuziba nafasi yake, japokuwa siwezi kuweka wazi ni nchi gani.

“Moja ya sababu zilizofanya tuachane naye ilikuwa ni hili la kuchelewa kurudi, japokuwa zipo sababu nyingine ambazo zimesababisha kufikia hatua ya kuachana naye.

“Alibakisha mkataba wa miezi nane, hivyo tumemalizana naye kwa kumlipa kila kitu na hatudaiani naye, tunaamini mchezaji tutakayemsajili atakuwa na kiwango kizuri cha kuweza kuziba nafasi yake ambaye atatua kabla ya Desemba 15 dirisha kufungwa,” alisema Tiboroha ambaye hakuwa tayari kuweka wazi wamemlipa kiasi gani, hata hivyo taarifa nyingine zinadai kuwa amelipwa Sh milioni 30.

Kanye West na Kim K Wataja Jina la Kichanga Wao na Vipimo Vyake
Wakenya Wamchenjia Kenyatta, Wamkaribisha Upya Kenya