Beki wa Liverpool Joe Gomez atakosa fainili za kombe la dunia zitakazoanza Juni 14 nchini Urusi, kufuatia majeraha ya kifundo cha mguu yanayomkabili kwa sasa.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 20 alimua kifundo cha mguu mwezi Machi akiwa katika majukumu ya timu ya taifa ya England, na siku kadhaa zilizofuata aliweza kucheza michezo ya ligi dhidi ya West Brom na Stoke City.
Gomez amefanyiwa vipimo katika jeraha hilo, na imebainika hatoweza kucheza mchezo wa fainali dhidi ya Real Madrid Mei 26, na atalazimika kufanyiwa upasuaji ili kufanikisha hatua ya kupona kwa haraka zaidi.
Tayari alikua katika mipango ya kocha mkuu wa timu ya taifa ya England Gareth Southgate ambaye amewahi kumtumia katika michezo kadhaa ya kimataifa ya kirafiki, na kuonyesha angemfaa katika fainali za kombe la dunia za mwaka huu.
Baada ya taarifa za kutakiwa kufanya upasuaji Gomez ameandika kwenye akaunti yake ya Instagram: “Inasikitisha, msimu wangu upande wa klabu umeishia hapa, na sitokua sehemu ya timu ya taifa itakayoshiriki fainali za kombe la dunia nchini Urusi, nitafanyiwa upasuaji hivi karibuni.
Kocha Southgate anatarajiwa kutaja kikosi cha timu ya taifa Mei 14, ambacho kitasheheni wachezaji 35, na Juni 04 atakipunguza na kufikia idadi ya wachezaji 23 ambao atasafiri nao hadi nchini Urusi.