Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewasilisha barua rasmi ya kujiuzulu nafasi hiyo.

Kupitia taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari, Ndugai amesema kuwa amewasilisha barua ya kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na amefanya hivyo kwa hiari na kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Pia, nakala ya barua yangu hiyo ya kujiuzulu nimeiwasilisha kwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya hatua stahiki kwa mujibu wa Katiba ya nchi na sheria nyingine husika ili kuwezesha mchakato wa kumpata Spika mwingine,” imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Ndugai.

Uamuzi wa Ndugai umekuja kukiwa na shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CCM na wabunge, wakimtaka kuchukua hatua hiyo, baada ya kuonekana akipinga hatua ya Rais Samia kuchukua mkopo wa Sh. 1.3 trilioni kutoka nje ya nchi. Katika kipande kilichosambaa mtandaoni, kilimuonesha akisema ‘ipo siku nchi hii itapigwa mnada’, kauli ambayo ilileta taharuki kubwa.

Wiki hii, Ndugai alimuomba msamaha Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania, lakini alieleza kuwa hakutoa kauli zenye lengo la kumpinga Rais na kwamba ujumbe ulihaririwa.

Akizungumza wakati wa kupokea taarifa ya matumizi ya fedha zilizotolewa kwa mkopo kwa lengo la kupambana na UVIKO-19, Rais Samia alionesha kushangazwa na kauli za Ndugai, akieleza kuwa ‘ni stress za 2025’.

Usikose kufuatilia uchambuzi wa tukio hili, hatua kwa hatua, kupitia YouTube Channel yetu ‘Dar24 Media’.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Januari 7, 2022
Zoezi la uokoaji Pemba lasitishwa