Jana Tarehe 27 Disemba 2021 Spika wa Bunge, Job Ndugai alihoji wanaofurahia nchi kukopa na kwamba deni limefika Sh70 trilioni
Akiwa katika mkutano mkuu wa pili wa wanakikundi cha Mikalile Ye Wanyusi uliofanyika jijini Dodoma, Spika wa Bunge Job Ndugai alitetea uamuzi wa Bunge kuanzisha tozo za miamala ya simu, kuliko kuendelea kukopa
“Sisi Watanzania wa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa na madeni au tubanane banane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa makubwa haya yasiyoeleweka, Ni lini sisi tutafanya wenyewe na kwa vipi” alisema Spika Ndugai
“Tukasema pitisha tozo anayetaka asiye taka pitisha tozo, lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia, yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha,” aliongeza.
Aidha, Ndugai alitoa mfano halisi akieleza kuwa Rais Samia alikwenda kukopa Trilioni 1.3 kwa ajili ya maendeleo, akieleza kuwa deni linavyozidi kupanda huenda ipo siku nchi itapigwa mnada.
“Sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo nayo sawa waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo ni namna ya kuongoza nchi, hivi sasa deni letu Sh70 trilioni… hivi nyinyi si wasomi je hiyo ni afya? Aliongeza Spika Ndugai.
Rais Samia Suluhu Hassan leo Tarehe 28 Disemba katika hafla ya kusaini mkataba wa SGR amesema ni lazima serikali ikope ili kumaliza miradi ya maendeleo.