Mabingwa wa kihistoria Tanzania Bara Young Africans leo walikuwa Bungeni huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akimuulizia mchezaji Bernard Morrison ambaye hata hivyo hakuwepo.
Wakati timu hiyo ikitambulishwa, wabunge mashabiki wa Young Africans walishangilia huku wale wa Simba wakiwa kimya.
Hata hivyo katika utambulisho huo, Spika Ndugai aliwapiga kijembe Young Africans, kwa kumuulizia Morrison ambaye hayumo na timu hiyo mkoani Dodoma huku sababu za kutosafiri na timu zikiwa hazijawekwa wazi.
“Waheshimiwa wanauliza mchezaji mmoja tu sijui Morrison naomba asimame. Morrison yupo, yupo eeeh, hayupo bwana, hayupo, hayupo naomba wale waheshimiwa wa Simba wapeni makofi kidogo,” alisema.
Kauli hiyo ya Spika ilionekana kuwakosha wabunge wa Simba ambao awali walikaa kimya wakati wa utambulisho wa wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi na viongozi kadhaa wa Young Africans ambao walitinga bungeni hapo.
Spika alisema licha ya Simba kufungwa katika mchezo uliopita lakini watakapokutana tena Simba itashinda.
“Mjiandae kisawasawa maana itarudi mikuki kadhaa,” alisema.
Hii sio mara ya kwanza kwa Bernard Morrison ambaye aliifungia Young Africans bao pekee la ushindi dhidi ya Simba katika mchezo ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu huu kutajwa bungeni kwani mara ya kwanza ilikuwa ni katika hotuba ya Waziri wa Fedha, Phillip Mpango alipokuwa akisoma bajeti ya serikali bungeni.
“Mheshimiwa Spika, mwisho, japo si kwa umuhimu Rais wetu ni mkakamavu na mpezni wa maendeleo ya michezo nchini,” alisema Dk Mpango na kuongeza kwenye kufungia hotuba yake kwa kusema;
“Mnamfahamu katika ubora wake, mazoezi ya push-ups anazopiga usiige! Mtamkumbuka pia jinsi alivyowaalika Ikulu Dar es Salaam vijana wetu wa timu ya taifa wenye umri chini ya Miaka 17 na makocha wao ili kuwajengea ari ya utaifa na kushinda.
Aidha, naamini hamjasahau siku Mhe. Magufuli alipokwenda Uwanja wa Taifa, kujiionea mpambano wa watani wa jadi, Young Africans na Simba na kushuhudia mnyama akipigwa mkuki mmoja wa sumu kali na Bernard Morrison!
Inaonekana Mheshimiwa Waziri Mkuu, na wewe Mheshimiwa Spika na hata Mheshimiwa Naibu Spika machale yaliwacheza mapema siku hiyo hamkuonekana uwanjani,” alisema Waziri Mpango.