Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema hali ya hewa ilivyo sasa inatia wasiwasi wa namna nchi zinavyoweza kukabiliana na changamoto hiyo ukosefu wa chakula.
Ndugai amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua Jukwaa la Wabunge kutoka nchi 10 za Mashariki mwa Afrika jijini Arusha leo Aprili 16, 2019 kuhusu usalama wa chakula na lishe.
Amesema kuwa hali ya kutonyesha mvua kwa wakati inaweza kusababisha Tanzania kuingia katika kipindi cha ukosefu wa chakula katika kipindi cha miezi sita ijayo.
“Lakini wakati tukiwa na changamoto hizi ambazo nyingine zinasababishwa na mabadiliko ya tabianchi kuna maeneo mengine katika ukanda wetu kuna chakula cha ziada lakini kutokana na kutokuwepo miundombinu mizuri ya barabara hakiwezi kuwafikia,” amesema Ndugai.
Amesema suala la ukosefu wa chakula halipaswi kufichwa kwa viongozi kushindwa kutoa taarifa za upungufu au ukosefu wa chakula kwa sababu linagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Ndugai amesema wakati Bunge la Tanzania lipo kwenye kikao cha bajeti ya mwaka 2019/20 jijini Dodoma, kama nchi imejidhatiti kuhakikisha inaipa umuhimu nafasi ya usalama wa chakula kwa kuunga mkono Azimio la Malabo linalotaka kila nchi za Afrika kutenga asilimia 10 ya bajeti yake kwenye kilimo.
“Tanzania tulikua na sera yetu ya Kilimo Kwanza si kwamba tumeitupa, kwa hiyo eneo la kilimo, mifugo na maji ni eneo linalopewa kipaumbele cha aina yake katika bajeti ya Serikali, kwa sababu bila kufanya hivyo ni hatari kwa usalama wa chakula kwa watu wetu,” amesema Ndugai.
Naye mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (Fao) nchini Tanzania, Fred Kafeero amesema jitihada za pamoja na uanzishwaji wa jukwaa la wabunge wanaohusika na kilimo litaweza kusukuma ajenda ya kuhakikisha sekta ya kilimo inatengewa fedha za kutosha ili kupiga vita utapiamlo.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Afrika Mashariki (Eala) inayohusika na Kilimo, Utalii na Maliasili, Mathias Kasamba amesema Azimio la Malabo la mwaka 2014 ambalo Marais wa Afrika waliweka mikakati ifikapo mwaka 2025 kusiwe na njaa Afrika kwa kutenga asilimia 10 kwa ajili ya kilimo kwenye bajeti zao.
Hivyo, mewaomba wabunge wenzake kuangalia kwenye bajeti za nchi zao ni kiasi gani nchi zao zimetenga kwenye bajeti ya kwa ajili ya kilimo na lishe kulingana na azimio la Malabo na muhimu kuwa na mfumo au utaratibu kufuatilia bajeti hizo akitoa mfano wa nchi ya Burundi iliyotenga asilimia 12 katika bajeti iliyopita.