Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kuwa amepokea taarifa ya kufanyiwa ukaguzi kwa ofisi ya CAG, Profesa Mussa Assad, ambao umefanywa na kampuni binafsi na yeye kuikabidhi kwenye kamati ya PAC na kueleza baada ya uchambuzi ataisoma taarifa hiyo bungeni.
Ameyasema Bungeni jijini Dodoma wakati wa muendelezo wa vikao vya Bunge la 11 jijini humo, ambapo amedai kuwa katika suala la ukaguzi hakuna taasisi inayolikwepa.
“Ningependa kuwajulisha juu ya taarifa ya ukaguzi wa ofisi ya CAG kwa mwaka fedha unaoshia Juni, 2018, hesabu za CAG zinapaswa kukaguliwa walau mara moja kwa mwaka, na Kamati ya PAC ndiyo inajukumu la kukagua ofisi hiyo, kazi imeshafanyika na imetuletea taarifa ya hesabu zilizokaguliwa za ofisi hiyo.”amesema Spika Ndugai
Aidha Spika Ndugai amesema kuwa taarifa ya kukaguliwa ofisi ya CAG, ameshaipitia na ameona kuna mambo, lakini kiutaratibu ameshaipeleka PAC na wakishamaliza uchambuzi watawasilisha kwake ili aweze kutoa taarifa kwani kwenye masuala ya ukaguzi hakuna anayebaki kila watu wanawakagua wenzao.
Hata hivyo, Spika Ndugai na CAG Prof. Assad wamekuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu kufuatia mara ya kwanza CAG akiwa nje ya nchi kutoa kauli ambayo ilionyesha kulidhalilisha Bunge la Tanzania kwa kudai kuwa Bunge hilo ni dhaifu.