Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kuwa ni haki ya kidemokrasia ya wabunge kutoka nje ya Bunge kwani hakuna kanuni inayowazuia kufanya hivyo.

Spika Ndugai aliyasema hayo katika mahojiano maalum katika kipindi cha Funguka cha Azam TV kilichorushwa jana.

Hata hivyo, Ndugai alisema kuwa ingawa ni haki kwa wabunge kufanya hivyo, tabia iliyooneshwa na wabunge wa vyama vya upinzani katika kikao cha Bunge kilichopita imezidi.

“Hakuna kanuni inayomkataza mbunge kutoka nje, ni sehemu ya demokrasia yao, lakini hii ya sasa imezidi, ni jambo lisilopendeza… maana watanzania wamewatuma kwenda kuwakilisha hoja zao, wanapotoka inakuwa haipendezi,”alisema.

Akizungumzia mvutano uliopo hivi sasa ndani ya Bunge hilo, alisema kuwa umetokana na kuendekeza kile alichokiita ‘uvyama’ zaidi na baadhi ya wabunge kuendekeza maslahi binafsi.

Aidha, alishauri kufanyika mazungumzo baina ya pande mbili ili kuondoa tofauti iliyopo hivi sasa ndani ya Nyumba hiyo ya wawakilishi.

“Nawaomba katika bunge lijalo kama wanahisi tunakosea watueleze, na sisi tuwaeleze wanakosea wapi ili twende sawa,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Spika Ndugai alikiri kupokea malalamiko ya Mbunge wa Chadema, James Ole Millya dhidi ya Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson akionesha kutokuwa na imani naye na kwamba baada ya kuiwasilisha kwenye Kamati husika, tuhuma hizo zimeonakana kutokuwa za kweli.

“Wabunge wa upinzani wanapitia changamoto nyingi kabla ya kuingia Bungeni, wengi wao wanahangaika sana kupata ubunge hadi kufikia hatua ya kulala sana selo (polisi) kwaiyo namna ya ‘kudeal’ nao inahitaji uvumilivu kidogo. Naibu Spika siyo mbunge wa jimbo, na wao wamezoea mbunge wa jimbo ambaye anafanana nao, Naibu Spika ni mbunge wa uteuzi kwahiyo wanahisi anafanya kazi kwa kufuata maelekezo kutoka nje ya bunge au anatumikia mabwana wawili jambo ambalo siyo kweli,” Ndugai anakakaririwa.

Katika hatua nyingine, aliwataka wabunge wa CCM kutotumia muda mwingi kuwarushia vijembe wabunge wa upinzani bali wajikite katika kujenga hoja.

 

CUF yampiga chini rasmi Profesa Lipumba
Spika Ndugai Afunguka,Aahidi Kukaa Chini Na Ukawa