Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Tanzania na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Emmanuel Gabriel lukula ameeleza juu ya kifo cha Salum Juma Kindamba mkazi wa Chanika aliyefariki dunia katika hospitali ya Temeke  mara baada ya kupigwa risasi ya kiunoni na mguuni na Polisi.

Kamanda Lukula amezungumza hayo kufuatia suala ambalo limekuwa likiongelewa katika vyombo vya habari mbalimbali juu ya ndugu wa marehemu huyo aliyeuawa mikononi mwa polisi kususa kuuzika mwili huo.

Ambapo ndugu hao wamesusa kuzika mwili huo kutokana na sintofahamu ya mazingira ya kifo cha ndugu yao ambaye alipigwa risasi na jeshi la polisi katika mkoa wa kipolisi Temeke.

Kamanda Lukula amesema kuwa marehemu, Salum Kindamba aliuawa na polisi katika harakati za kukamata majambazi walioripotiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Chang’ombe eneo la Kiwalani ambapo iliripotiwa kuwa watu wanne wasiofahamika wamefika katika eneo hilo wakiwa na silaha aina ya Pistol.

Hata hivyo kumekuwapo na taarifa juu ya matukio ya ujambazi katika maeneo tofauti katika mkoa wa kipolisi Jijini Dar es salaam, kufuatia matukio hayo ya ujambazi yaliyoripotiwa Kamanda Mkuu kanda maalumu ya Dar aliamuru kuundwa kikosi kazi cha kudhibiti matukio hayo.

Hivyo mara baada ya kusikia taarifa juu ya majambazi hao katika eneo la kiwalani kikosi kazi kilihamia huko kupambana na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne na mfuko wenye silaha.

Dakika chache mara baada ya kuwatia mbaroni watuhumiwa hao akiwemo, Salum Kindamba alikurupuka na kufanikiwa kutoroka na mfuko ule wenye silaha aina ya pistol, pesa taslimu Sh. milioni 9 na simu aina ya Tecno.

Polisi walifanya jitihada zote kisheria kumtaka kijana huyo asimame bila kudhuliwa jitihada hizo ziligonga mwamba ndipo Polisi walipoamua kumpiga risasi ya kiunoni na  mguuni na kumkamata kijan huyo ambaye baadae alikimbizwa hospitali ya Temeke na kufariki dunia.

Taarifa hiyo imetolewa leo Agosti 22, 2018 kwenye vyombo vya habari kufuatia sintofahamu kwa ndugu wa marehemu ambao walikuwa hawafahamu kiundani juu ya mazingira yaliyopelekea ndugu yao kufikwa na mauti akiwa mikononi mwa polisi.

Video: DC Daqaro awafunda madereva Arusha
Video: Tunamtambua Prof. Lipumba, Maalim Seif amesimamishwa- Mwinyi