Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amesema
kuwa Serikali kupitia Wizara yake inashirikiana na wadau wa sekta ya mawasiliano
kuhakikisha inatatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ili wananchi waweze kupata
huduma bora za mawasiliano kwa gharama nafuu katika maeneo yote nchini.
Ndugulile amebainisha hayo katika kikao chake cha majadiliano na Watendaji Wakuu wa
makampuni ya simu Tanzania kilichofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma
kwa lengo la kutatua changamoto na kuwa na mkakati wa pamoja wa kuongeza wigo wa
mawasiliano ya kasi ya simu na data nchini.
Ndugulile amesema kuwa matamanio ya Serikali ni wananchi wake kuweza kutumia
mawasiliano ya simu na data kufanya biashara mtandao, kupata huduma mbalimbali za
Serikali kwa njia ya mtandao na kushiriki katika kuinua uchumi wa kidijitali.
“Tumefanya kikao cha ndani na Watendaji Wakuu wa makampuni ya simu na kuongelea
masuala ya vifurushi na bando, suala hili tunalifanyia kazi kwa pamoja na hivi karibuni
Serikali itatoa kauli kuhusiana na masuala ya vifurushi,”, amesema Ndugulile.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na watoa huduma za
mawasiliano nchini kwa kuhakikisha inatengeneza mazingira wezeshi na kutatua
changamoto zinazojitokeza katika sekta ya mawasiliano.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Zainab Chaula alisema kuwa Serikali imewekeza
katika TEHAMA ili kuwezesha na kuboresha uzalishaji na uendeshaji wa sekta takribani zote
nchini, na kuwataka wadau wa sekta ya mawasiliano kutembea pamoja ili kutimiza malengo
ya Serikali ya kuipeleka nchi katika mapinduzi ya nne ya viwanda na uchumi wa kidijitali.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Justina Mashiba amesema
mfuko huo umeratibu kikao hicho cha wadau wa mawasiliano ikiwa ni agizo la Waziri,
ambapo moja ya ajenda ni kufanya majadiliano ya namna bora ya kufikisha huduma za
mawasiliano katika maeneo ya vijijini na mipakani kwa kutumia teknolojia bora na rahisi.