Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Faustine Ndugulile amesema kuwa serikali imepanga kuchukua hatua kali dhidi ya wale watakaobainika kupotosha mma na kutoa taarifa ambazo zinazua taharuki kwa wananchi.
Ndugulile ametoa onyo hilo wakati akizungumza na Dar24 katika jijini Dar es Salaam baada ya kuulizwa hatua ambazo serikali imepanga kuchukua kufuatia wimbi la watu wanaosambaza taarifa za uongo mitandaoni nyingi zikihusu magonjwa na vifo, taarifa ambazon zinazua taharuki kwa wananchi.
“Niwahakikishie tumekubaliana ndani ya serikali, kuanzia sasa, mtu yeyote tutakayembanini anatoa taarifa zozote za uchochezi, za upotoshaji, kwa kweli tutachukua sheria kali na watu wasije wakatulaumu, nadhani kuanzia sasa mtaanza kusikia,” amsema Ndugulile.
Akizungumzia suala la watu wanaotuma jumbe za kuomba kutumiwa hela kwa kutumia namba ngeni na kutapeli watu Waziri Ndugulile amesema linafanyiwa kazi na Serikali imepanga kuanza kutoa elimu kwa umma kuhusiana na utapeli na masuala mbalimbali yanayohusu jinai katika mtandao.
Aidha Waziri Ndugulile amesema ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA kuhakikisha watu wote nchini wanahakiki usajili wa namba zao za simu na kwamba wale wote watakaokiuka kufanya hivyo ndani ya muda uliopangwa namba zao zitafungiwa.