Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amekutana na Menejimenti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknojia ya Habari akiambatana na Naibu wake Mhandisi Kundo Andrea Mathew kwa lengo la kufahamiana na kutoa maagizo juu ya utendaji kazi ili Wizara hiyo mpya isimame na kuchukua nafasi yake katika utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi.

Akizungumza na Menejimenti kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara uliopo Mji wa Serikali Mtumba, Dkt. Ndugulile amewataka watendaji wasisubiri kuagizwa, wafanye kazi kwa bidii ili kabla ya kuulizwa wawe wamejiongeza na kutekeleza.

Ndugulile amesema kuwa, Wizara hiyo ni mtambuka, ya kimkakati na kiuchumi na inagusa Wizara zote na maisha ya kila mtanzania, ina nafasi kubwa na muhimu katika kuchangia pato la Taifa na kukuza uchumi wa nchi.

“Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha Wizara inasimama na kuchukua nafasi yake, sisi ndio wenye sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016, sheria, kanuni na miongozo mbali mbali hivyo tunaenda kugusa Wizara takribani zote zinazotumia miumboninu na mifumo ya TEHAMA na huduma za mawasiliano katika utoaji huduma na ukusanyaji wa kodi za Serikali,” amesisitiza Ndugulile.

Aidha, amewataka watendaji wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii huku wakitekeleza masuala yanayohusu Wizara hiyo mpya kama yalivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 pamoja na yaliyopo kwenye hotuba ya Rais wa Tanzania Dkt. John Joseph Magufuli wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba mwaka huu.

Mambo ya nje wamhakikishia ushirikiano Olenasha
Dkt. Gwajima awataka Viongozi Wizara ya Afya kuongeza ufanisi