Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Suleiman Yamin Ndikumana amemtetea mchezaji mwenzake wa zamani wa klabu hiyo Juma Said Nyosso kwa adhabu aliyopewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Nahodha wa Mbeya City, Nyosso jana amefungiwa kucheza soka kwa miaka miwili pamoja na kutozwa faini ya Sh, Milioni 2 kwa kosa la kumdhalilisha, Nahodha wa Azam FC, John Raphael Bocco.

Tukio hilo lilitokea Jumapili kipindi cha kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya wenyeji Azam FC na Mbeya City Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

“Miaka miwili ni mingi sana, sasa wanategemea aishi vipi na familia yake wakati mpira ndiyo kazi yake?”alihoji Ndikumana akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE usiku wa jana.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Burundi, ambaye kwa sasa anachezea Primeiro de Agosto ya Angola amekuwa mchezaji pekee kumtetea Nyosso, baada ya wengi kushinikiza apewe adhabu kali.

Kwani hiyo imekuwa mara ya nne kwa Nyosso kuonekana akifanya hivyo uwanjani, mara ya kwanza akiwa Ashanti United mwaka 2007 alimfanyia hivyo mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Jospeh Kaniki aliyejibu kwa kumpiga ngumi hali iliyomponza kufungiwa na TFF.

Akarudia tena mwaka 2010 alipomfanyia beki wa zamani wa Yanga SC, Amir Maftah ambaye alijibu kwa kumpiga kichwa akatolewa kwa nyekundu, na msimu uliopita akiwa Mbeya City, alipomtomasa aliyekuwa mshambuliaji wa Simba SC, Elias Maguri. Kutokana na ushahidi wa picha za magazeti, Nyosso alifungiwa mechi sita na TFF.

Huku wengi wakidhani kwamba adhabu hiyo itakuwa fundisho kwake na hataweza kurudia tena, lakini Jumapili Nyosso ameonyesha yeye ni ‘nunda’, kwa kurudia tena baada ya kumdhalilisha Bocco.

Chanzo; Bin Zubeir

 

Kitendo Hiki Kimemsikitisha Lowassa
Mourinho Awashangaza Waandishi Wa Habari