Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro anaendelea na ziara ya siku sita (6) katika maeneo ya mipaka iliyopo mkoani Ruvuma.
Mpaka sasa mefanya ziara katika mpaka wa Wenje uliopo Wilayani Tunduru, Chiwindi uliopo Wilayani Nyasa na mpaka wa Magazini uliopo Wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma. Mipaka hii inaiunganisha Tanzania na Nchi jirani ya Msumbuji.
Ziara hii ambayo inatokana na utekelezaji wa majukumu ya Wizara, ikiwemo utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, kujenga, kulinda na kudumisha uhusiano wa kimataifa, inalenga kuwahimiza watendaji na Mamlaka mbalimbali za Mkoa na Wilaya za Mipakani kuhusu umuhimu wa wakudumisha, kulinda, na kuendeleza uhusiano mzuri baina ya Taifa letu na nchi tunazo pakana nazo.
Kadhalika, ziara hii inalenga kuhimiza umuhimu wa kulinda mipaka ya nchi na kubaini changamoto zinazowakabili wakazi wa mipakani
Dkt. Ndumbaro amewataka watendaji na Wakuu wa Wilaya hizo, kuendelea kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, vilele kutengeneza na kuanzisha masoko ya bidhaa mbalimbali maeneo ya karibu na mipakani kwa lengo la kuchagiza biashara, ajira na kuongeza mapato ya Serikali.
“Wizara tumejipanga kutekeleza mkakati wa kuhakikisha kuwa tunashiriana kwa ukaribu na wadau wanaosaidia kutekeleza majukumu ya Wizara zikiwemo Mamlaka za Mikoa na Wilaya ambazo zipo mipakani” amesema Dkt. Ndumbaro
Wakati huo huo katika ziara hii Dkt. Ndumbaro amekutana na kufanya mazungumzo na kamati za ulinzi na usalama katika Wilaya ya Namtumbo ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Julius Mtatiro na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nayasa ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Isabela Chilumba.
Wakuu wa Wilaya zote tatu pamoja Wakuu vya Vyombo vya Ulinzi na Usalama wa Wilaya hizo kwa nyakati tofauti waliambatana na Dkt. Ndumbaro kuzuru maeneo ya Mipakani.
Wananchi wa Tunduru kwa upande wao wameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mshariki kwa kuwatembelea na kusikiliza changamoto zinazo wakabili.
Baadhi ya changamoto walizozitaja ni pamoja na kutokuwepo kwa huduma ya kivuko cha uhakika, barabara (kiwango cha lami) ukosefu wa huduma ya maji safi na salama ya uhakika na umeme. Hata hivyo Dkt. Ndumbaro ameeleza hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali kutatua changamoto hizo.