Waziri wa Sheria na Katiba, Damas Ndumbaro amesema malalamiko 1524 yaliyohusu uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora yaliwasilishwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB).
Waziri Ndumbaro ameyasema hayo hii leo Aprili 25,2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara yake ambapo amesema hadi kufikia Julai Mosi, 2022, THBUB ilikuwa na jumla ya malalamiko 1,524.
Amesema, kati ya hayo, malalamiko 725 yalihusu haki za binadamu na malalamiko 799 yalihusu utawala bora.
“Kati ya mwezi Julai 2022 hadi Machi, 2023, THBUB ilipokea malalamiko mapya 123. Kati ya hayo, 39 yalihusu haki za binadamu na 84 yalihusu utawala bora.”Amesema
Aidha, amesema katika kipindi hicho malalamiko yaliyofungwa yalikuwa 719, yote ya miaka ya nyuma kati ya hayo, malalamiko 318 yalikuwa ya haki za binadamu na 401 ya utawala bora.
Hivyo kufanya idadi ya malalamiko yanayoendelea na uchunguzi katika hatua mbalimbali kuwa 928 kati ya hayo, malalamiko 446 yalikuwa ya haki za binadamu na 482 ya utawala bora.