Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevihimiza vyama vya siasa kutoa elimu ya mpiga kura kwa wapiga kura na wanachama wao bila ya kuegemea itikadi ya vyama vyao kwani sio wote wanao waelimisha ni wanachama wao.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Emmanuel Kawishe, wakati akitoa elimu ya mpiga kura kupitia kituo cha Redio kilichopo mjini Bukoba.

Amesema mdau namba moja wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni chama cha siasa na kwamba NEC inakutana na vyama hivyo mara kwa mara kushauriana namna ya kutoa elimu ya mpiga kura na namna ya kuwafikia wananchi wengi.

“Kwa hiyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavihimiza vyama vya siasa kutoa elimu ya mpiga kura kwa wapiga kura na kwa wanachama wao pia, tena tunawasihi vyama vya siasa wasitoe elimu kwa njia ya itikadi za kichama watoe elimu isiyoegemea itikadi yoyote kwa sababu kuna wengine sio wanachama wa chama chake lakini watawapigia kura,”amesema Kawishe.

Aidha, Kawishe amefafanua kuwa pamoja na kuvikumbusha vyama vya siasa wajibu wao katika kutoa elimu ya wapiga kura, vyama hivyo vimekuwa vikitoa ushirikiano mzuri katika kutoa elimu hiyo.

Vile vile amesema kuwa asilimia kubwa ya vyama hivyo vilitoa elimu ya mpiga kura na kuelimisha wananchi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na ndio maana mwitikio wa wapiga kura kupiga kura ulikuwa mkubwa ikilinganishwa na chaguzi zilizopita.

Hata hivyo, Kawishe amesema pamoja na kutoa fursa hiyo kwa vyama Tume haikusita kuvirekebisha pale ambapo vilikosea katika kutoa elimu ya mpiga kura.

Kwa sasa Tanzania ina vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu kutoka vyama 22 vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 baada ya vyama vitatu kufutiwa usajili na Msajili wa Vyama vya Sisasa mwaka jana 2016.

 

Mamelodi Sundowns Wanogewa Na Denis Onyango
Paul Biya Awapongeza Wachezaji Wa Cameroon