Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima amesema changamoto kubwa inayoikabiri tume hiyo kwa sasa ni utoaji wa elimu ya mpiga kura.
Amesema kuwa ukosefu wa elimu hiyo unawafanya baadhi ya wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani ambao wanaingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi bila kufahamu mfumo wa uchaguzi nchini.
Aidha, amesisitiza kuwa viongozi na wanachama wa vyama hivyo kufuatilia vipindi na taarifa mbalimbali zinazoelekeza taratibu za uchaguzi ili kuzielewa na kuepuka upotoshaji kuhusiana na uendeshaji wa uchaguzi.
Vile vile ameongeza kuwa, hali hiyo inakwenda hata katika ngazi za Mahakama ambapo mtu akishinda kesi anasema Mahakama iko huru,lakini akishindwa anasema Mahakama haiko huru.
Hata hivyo, Kailima amesema NEC ni mojawapo ya Tume inayotekeleza majukumu yake kwa uwazi zaidi ikilinganishwa na Tume nyingine za Uchaguzi katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la sahara na kwamba inapaswa kutazamwa kwa namna inavyotekeleza majukumu yake na si uteuzi wa watendaji.