Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeongeza siku mbili zaidi za kuapisha mawakala wa vyama vya siasa watakaosimamia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano ya wiki ijayo Oktoba 28, 2020.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dkt. Wilson Mahera akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam amesema, tume imeongeza muda huo kuwa hadi Oktoba 23 2020.

“Tume imeamua hivyo baada ya kubaini baadhi ya maeneo kuna changamoto ya kufikika kutokana na jiografia,” amesema Dkt. Mahera.

Shughuli ya uapishaji mawakala ilikuwa ifanyike kwa siku moja (yaani jana Jumatano) lakini katika maeneo mbalimbali, kumekuwapo na taarifa kutoka kwa vyama vya siasa na wagombea kulalamikia mawakala wao kutoapishwa.

Hata hivyo, Dk. Mahera amesema, watakaoapishwa katika kipindi hicho ni yale majina yaliyowasilishwa na vyama yakiwa na majina yenye namba za simu na yaliyopangwa kwa kila wakala atasimamia eneo gani.

Wanamgambo 19 wa Al-Shabaab waangamizwa
BASATA yakanusha kuufungia wimbo wa Jide