Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa ufafanuzi kuhusu ongezeko la wapiga kura milioni moja waliodhihirika baada ya mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Damian Lubuva kutangaza matokeo, idadi ambayo ilizidi idadi ya majina ya wapiga kura waliokuwa kwenye daftari walilowapa vyama vya siasa.

Awali, Tume ya Taifa ilieleza kuwa ilifanya uhakiki katika daftari la kudumu la mpiga kura kwa wapiga kura waliojiandikisha kwa njia ya BVR, na kufuta majina ya watu milioni moja. Zoezi hilo lilipelekea majina ya wapiga kura kupungua kutoka milioni 23 hadi milioni 22 ambayo ilipatikana kwenye daftari lililogawiwa kwa vyama vya siasa.

Hata hivyo, utata uliibuka wakati Mwenyekiti wa Tume hiyo akitangaza matokeo na kueleza kuwa idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ilikuwa milioni 23 tofauti na milioni 22 iliyokuwa kwenye daftari walilowapa vyama vya siasa.

Akifafanua utata huo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari wa NEC, Clarence Nanyaro alieleza kuwa idadi ya watu iliongezeka katika siku za mwisho za kupiga kura baada ya watu waliokuwa wamejiandikisha kubaini kuwa majina yao hayakuwa katika kumbukumbu ya Tume hiyo.

Alieleza kuwa kutokana na muda, hawakuweza kuwapa vyama vya siasa daftari lenye orodha hiyo mpya.

“Tulifanya uhakiki siku za mwisho karibu na uchaguzi na kubaini kulikuwa na watu wengi ambao majina yao yalikuwa hayaonekani,” Nanyaro aliliambia gazeti ya Mwananchi.

Nicki Minaj Ashambuliwa Baada ya Kupost Picha Hii ya Ubakaji
Kukamatwa Watumishi Kituo Cha Sheria Na Haki Za Binadamu Kwazua Utata