Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kikao chake cha tarehe 12 Oktoba, 2020 imefanya maamuzi ya kisera ya kuruhusu vitambulisho mbadala kutumika kupigia kura.

Vitambulisho mbadala ambavyo mpiga kura anaruhusiwa kutumia ni Kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na NIDA, Hati ya kusafiria na Leseni ya Udereva. Hata hivyo, ni sharti majina yaliyoko kwenye vitambulisho hivyo yafanane na majina yaliyomo kwenye daftari la Kudumu la Wapiga kura katika kituo husika cha kupigia kura.

Uamuzi huo umezingatia matakwa ya Kifungu cha 61 (3) (a) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 ambavyo vinaipa Tume/Mkurugenzi wa Uchaguzi mamlaka ya kuruhusu kutumika kwa utambulisho mwingine wowote utakaomsaidia mpiga kura aliyejiandikisha kuweza kupiga kura iwapo amepoteza kadi yake ya mpiga kura ama imeharibika.

Tume imefanya uamuzi huo ili kuwawezesha wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao za kupigia kura au kadi zao zimeharibika, kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura Siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020.


Kiongozi wa upinzani ajitangaza mshindi kabla ya matokeo
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Oktoba 20, 2020