Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia Mkurugenzi wake, Ramadhani Kailima wameshangazwa na viongozi wa Chadema wanaosema hawatambui uteuzi wa Joseph David Njumbe kuwa mgombea wa ubunge jimbo la Singida Kaskazini.
Ramadhan Kailima ameeleza kuwa Chadema kupitia Katibu wa Wilaya wa Singida Vijijini wamekamilisha mchakato wa utambulisho wa mgombea wa Ubunge jimbo la Singida Kaskazini, Joseph Njumbe.
Ambapo Halmashauri ya Wilaya Singida iliteua wagombea 6 mmojawapo akiwa Joseph Njumbe wa Chadema, baada ya kuona amekidhi sheria, kanuni na vigezo vya katiba na chama chake cha Demokrasi na maendeleo (Chadema).
-
Msando alamba dili CCM
-
Magazeti ya Tanzania leo Desemba 21, 2017
-
NEC: Hakuna chama kilichojitoa kwenye mchakato wa uchaguzi
Hata hivyo Njumbe, aliwasilisha barua yake ya utambulisho iliyosainiwa na katibu wa Chadema wa Wilaya ya Singida Vijijini, Amani Mloya.
“Kwa hiyo wanapolalamika kwamba huyu hawamjui nawashangaa sana. Nawashangaa sana kwa saababu Kwa mujibu wa ibara ya 67 ibara ndogo ya 1b ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema Mgombea yeyote wa ubunge lazima awe amependekezwa na chama cha siasa kilichosajiliwa.” Amesema Kailima.
“Kanuni namba 31 kanuni ndogo ya kwanza ya uchaguzi wa Rais na wabunge ya mwaka 2015, inasema mtu akitaka kugombea ubunge atawasilisha barua yake ya utambulisho iliyosainiwa na katibu wa chama au wa wilaya wa chama husika. Barua yake inawasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi.”
Aidha, Kailima ameeleza kuwa Joseph Njumbe, pamoja na kuwa ameshakamilisha taratibu za kupitishwa kuwa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CHADEMA, bado ana haki ya kikatiba ya kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho pale tu atakapotimiza taratibu zinazotakiwa ili kujiondoa.
CHADEMA pamoja na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vilitangaza kutokushiriki uchaguzi huo mdogo wa wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Januari 18, 2018 ikidai kuwa mwenendo wa hali ya kisiasa nchini siyo shwari na kuitaka Tume ya uchaguzi kuahirisha uchaguzi huo.