Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wagombea na Vyama vya Siasa vinavyoendelea na kampeni za Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Madiwani kufanya kampeni za kistaarabu zinazozingatia maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015 na kwamba Chama au mgombea atakayekiuka maadili hayo atachukuliwa hatua.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mkuu Mstaafu Hamid M. Hamid zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi huo Januari 22, 2017 kufuatia baadhi Vyama na Wagombea kuanza kukiuka Maadili na taratibu za Kampeni  kwa kutoa matamko yaliyo nje ya Sera za Vyama vyao.

Aidha,amesema kuwa kipengele cha 2.1 (m) cha Maadili ya Uchaguzi kinaeleza  Wajibu wa Vyama vya Siasa na Wagombea katika kuendesha shughuli za Siasa wakati wa Kampeni kinavitaka Vyama vya Siasa, Wagombea na Wafuasi wao kufanya kampeni kwa kuzingatia misingi inayolenga kutangaza Sera ambazo hazijengi chuki, mafarakano na kuleta mgawanyiko katika jamii.

“Katika Kampeni zinazoendelea, baadhi ya vyama vya Siasa vimeanza kukiuka taratibu za kampeni na maadili na kutumia fursa ya kampeni vibaya, vinawasema viongozi wa Kitaifa , kutoa matamko ambayo kihalisia siyo ya kumnadi mgombea na kufanya kampeni zisizo za kistaarabu,” Amesema Jaji Hamid.

Amesema kuwa  Vyama au Wagombea watakaoendelea kukiuka Maadili ya Uchaguzi katika Mikutano ya kampeni inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Tanzania pamoja na Jimbo la Dimani, Zanzibar watachukuliwa hatua.

 

Rais Magufuli apokea ujumbe kutoka kwa rais wa Nigeria
Nikki: Wasanii wekezeni katika elimu