Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage ametangaza ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu kwa nafasi za urais, ubunge na udiwani ambapo kwa nafasi ya urais fomu zitaanza kutolewa Agosti 5 hadi 25, 2020 jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 23, 2020, jijini Dodoma Jaji Kaijage amesema kwa upande wa fomu za kuwania ubunge na udiwani zitatolewa Agosti 12 – 25 katika ofisi za wasimamizi wa uchaguzi za halmashauri za wilaya na makao makuu ya kata.
Amesema uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 25 Agosti, 2020 na kampeni zitaanza tarehe 26 Agosti hadi 27 oktoba 2020.
Kwa upande wa majimbo amesema hakutakuwa na nyongeza ya majimbo hivyo yatabaki yaleyale 264 ya mwaka 215, ambapo Tanzania bara majimbo 214 na Zanzibar majimbo 50.
Amebainisha kuwa kumefanyika mabadiliko ya majina katika majimbo matatu ambayo ni Chilonwa la mkoa wa Dodoma kuwa Chamwino, Jimbo la Mtera kuwa Mvumi na Jimbo la Kijitoupele la Zanzibar kuwa Pangawe.
Ikumbukwe kuwa jana Julai 22, 2020 Rais Dkt. John Magufuli wakati akizindua makao makuu ya NEC Dodoma alipendekeza jina la Jimbo la Chilonwa kuitwa Chamwino.
Kwa upande wa kata, jumla ya kata 3,956 za Tanzania bara zitafanya uchaguzi wa madiwani wa mwaka 2020.