Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka Wasimamizi wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika Septemba 16 mwaka huu katika Majimbo ya Ukonga na Monduli na kwenye Kata 13 za Tanzania Bara kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria na Kanuni zinazosimamia uchaguzi huo.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage wakati akifungua mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi wa Kata na Majimbo hayo.
Jaji Kaijage amewataka Wasimamizi hao kuzingatia weledi na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ili wapunguze na kuondoa malalamiko yanayojitokeza wakati wa uchaguzi.
Aidha, amesema kuwa uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa akisisitiza kwamba hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri wenye ufanisi usio na malalamiko au vurugu.
“Tunakutana hapa kwa muda wa siku tatu (3) ili kwa pamoja tubadilishane uzoefu, tujadili namna ya kufanikisha zoezi la uchaguzi lakini pia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi,” Amesema Jaji Kaijage
-
Makonda awaonya watakaonunua makontena yake
-
Lugola amsweka ndani mkuu wa kituo cha Polisi
-
Mpango apangua laana za Makonda, ‘Vitisho vya wanasiasa’