Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steve Kiruswa amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida Chone Malembo kuhakikisha wanakutana kabla ya Januari 30, 2022 ili kujadili namna ya kuutatua mgogoro wa wachimbaji wadogo wa eneo la Mkombozi ulio dumu kwa muda mrefu.
Pia amewaagiza Maafisa Madini waliopo katika Ofisi ya Afisa Madini wa Mkoa wa Singida kuhakikisha wanawatambua wachimbaji wadogo wa madini na kuwaelekeza mbinu bora za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Aidha Utekelezaji huo, inaelezwa kuwa ni moja ya jukumu la Wizara la kuhakikisha inawatambua na kuwarasimisha wachimbaji wadogo wa madini ili wachimbe kwa faida na watoke uchimbaji mdogo kwenda wa kati na hatimaye uchimbaji mkubwa.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri katika ziara yake ya kikazi mkoani Singida ambapo amesema Wizara yake inaendelea na jitihada za kuwatambua na kuwarasimisha wachimbaji wadogo wa madini kote nchini.
“Naomba nichukue fursa hii kuwataka watumishi wote wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi yaa Mkoa wa Singida kuwa wabunifu katika utendaji kazi wenu ili muweze kuwasadia wachimbaji wa Mkoa huu na kutafuta njia rafiki za ukusanyaji wa maduhuli ya serikali,” Amesema Dkt. Kiruswa.
Pia, Kiruswa ametembelea mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini ya dhahabu wa Sunshine Mine pamoja na mgodi wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wa Mkombozi uliopo katika kijiji cha Konkilangi Kata ya Sekenke wilayani Iramba mkoa wa Singida ili kukagua shughuli za uchimbaji madini na kusikiliza changamoto za wachimbaji wa maeneo hayo.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kiruswa ameipongeza Kampuni ya Sunshine Mine kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Kampuni hiyo na kuitaka ihakikishe inawaajiri wanawake wanaohitaji kufanya kazi migodini ili waweze kufaidika na shughuli za uchimbaji madini.
Sambamba na hayo, Dkt. Kiruswa amewahakikishia wawekezaji wa Sunshine Mine usalama katika uwekezaji wao na kuwaahidi ushirikiano pindi wanapokuwa na uhitaji kutoka Wizara ya Madini.