Boniface Gideon – Tanga
Shirika la Next Einstein Forum – NEF, kwa kushirikiana na kituo cha Sayansi Tanga cha Stem Park pamoja na Halmashauri ya jiji la Tanga limetoa tuzo kwa walimu 10 wa kike wa Shule za Msingi na Sekondari waliofanya vizuri katika ufundishaji wa masomo ya Sayansi na hisabati hii ikiwa na lengo la kuongeza motisha ya ufundishaji ili kuandaa wanafunzi mahiri watakaoingia kwenye soko la kiushindani wa ajira pamaoja na wataalamu mbalimbali wa baadaye.
Tuzo hizo zimekabidhiwa leo june 23,2023 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Tanga Dkt.Sipora Liana kwa walimu watano wa Shule za Msingi na watano wa Shule za Sekondari.
Akizungumza Wakati wa utoaji wa tuzo Dkt. Liana aliwapongeza walimu hao kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma yanayoendana sambamba na malezi bora kwa watoto huku akiwataka kuwa mabalozi kwa walimu wengine kwaajili ya kuandaa taifa lenye watu wema ,waadilifu na wenye kusimamia maadili mema.
Aidha Mkurugenzi huyo amewapongeza NEF pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo hasa katika sekta ya elimu kwa jitihada wanazoendelea kuzifanya kwaajili ya kuhakikisha kiwango cha taaluma kinakuwa kwa kuweka miundo mbinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madarasa , madawati pamoja na kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia.
“Hongereni sana walimu wote hasa walimu wa sayansi kwa kazi kubwa mnayofanya katika kutimiza wajibu wenu wa kuwafundisha watoto wetu na kuwaandaa katika misingi bora mnafanya kazi kubwa sana mnahitaji pongezi endeleeni kuwapa motisha watoto wetu, tunawapongeza sana wadau wote ambao tunasaidiana nao hasa kupitia sekta ya elimu kwa kujenga na kuboresha miundominu mbalimbali ya elimu “ alisema Dkt. Liana.
Akizungumza balozi wa shirika la Next Einstein Forum (NEF) Dkt. Isaya Ipyana alisema kuwa tuzo hizo walizozitoa kwa walimu wa kike wanaofundisha masomo ya sayanasi katika shule za msingi na sekondari ni katika kuwaongezea ari ya ufundishaji ili kuongeza ufanisi pamoja na kuwaandaa wanafunzi wenye uwezo mkubwa kitaaluma.
Dkt Ipyana aliwataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwalea watoto katika misingi bora ya kimaadili sambamba na kuwapa nafasi ya kupenda kujifunza masomo ya sayansi ambayo yana nafasi kubwa ya ajira katika ulimwengu wa sasa.
“Tuzo hizi zilizoandaliwa na NEF kwa kushirikiana na kituo cha sayansi cha Stem Park pamoja na halamashauri ya jiji la Tanga ni kwaajili ya kuwapatia motisha walimu wa kike wanaofundisha masomo ya sayansi na hisabati katika shule za msingi na sekondari , niwaase sana wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika mazingira bora na kupenda kujifunza masomo ya sayansi kwani ndio yenye tija katika ulimwengu wa sasa unaoenda kidigital.” alisema Dkt. Ipyana.
Awali akizungumza afisa maendeleo ya jamii Simon Mdende amesema pamoja na jitihada mbalimbali wanazozifanya walimu kupitia sekta ya elimu ni vyema wakatambua kuwa wanalo jukumu kubwa la malezi kwa watoto pindi wanapokuwa mashuleni katika kuhakikisha wanasimamia maadili mema pamoja na kuwaepusha na vitendo vya ukatikatili
“Pamoja na kuwa walimu mnafanya vizuri kitaaluma katika masomo hasa ya sayansi lakini nisistize kwamba ulimwengu wa sasa umebadilika sana naomba tuhakikishe tunawalea watoto wetu katika maadili mazuri , tuwakinge na maadili mabaya yanayopelekea mmomonyoko wa maadili hasa maswala ya ukatili wa kijinsia” alisema Mdende.