Serikali imejipanga kuhakikisha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, NEMC na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar – ZEMA, zinapata usajili Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi – GCF.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Azani Mwinyi aliyeuliza hatua za kusajili taasisi kwenye Mfuko wa GCF, bungeni jijini Dodoma leo Novemba 10, 2023.
Amesema kuwa hatua zinazofanyika ni kuwa taasisi mbalimbali zenye nia ya kusajiliwa zinawasilisha maombi katika Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ndiyo mratibu kisha mchakato unaenda GCF inaratibu zikikidhi vigezo zinapata usajili.
Dkt. Jafo amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea na mawasiliano, majadiliano na mazungumzo ya kuhakikisha usajili kwa taasisi za Serikali unakamilika.
“Kwa sasa kwa sasa zaidi ya taasisi sita bado hazijafanikiwa kwahiyo tunaendelea kufanya kazi ya kuwahamasisha wenzetu wa Mfuko ili wakubali maombi yetu kwa lengo sasa taasisi zetu ziweze kunufaika,” amesema.
Aidha, Waziri Jafo amefafanua kuwa NEMC tayari imeshaomba na kuanza mchakato wa usajili tangu mwaka 2021 na upande wa ZEMA ilikuwa bado hajawasilisha maombi ya usajili kwenye Mfuko wa GCF.