Siku moja, Thomas Alva alirudi nyumbani na kipande cha karatasi mkononi akamkabidhi mama yake huku akimwambia: “Mwalimu amenipa barua hii, na kunisisitiza nimkabidhi Mama yangu.”
Macho ya mama yake yalitota machozi kadri alivyokuwa akiisoma barua ile na baada ya kujifuta machozi, alitabasamu huku akimpapasa kichwa mwanaye.
Kisha akamsomea kwa sauti barua ile: “Kwa mzazi wa Thomas, mtoto wako ana akili nyingi mno (genius), ila kwa bahati mbaya Shule yetu ina vifaa dhaifu na Walimu wenye uwezo mdogo kumfundishia mwanao, tafadhali mfundishie wewe mwenyewe tu Nyumbani.”
Thomas alifarijika kwamba, yeye ni mtoto mwenye akili nyingi licha ya kuwa aliondolewa Shuleni. Lakini baadaye miaka mingi baada ya Mama yake kufariki, Thomas aliondokea kuwa Mfanyabiashara mkubwa na mwenye akili nyingi.
Siku moja, Thomas aliperuzi makablasha ya zamani ya marehemu Mama yake, akaiona ile barua aliyokabidhiwa na Mwalimu, aliifungua na kukuta ujumbe huu: (Kwa mzazi wa Thomas, mtoto wako ni mgonjwa wa akili. Hatumruhusu tena kuendelea na masomo katika shule yetu. Unaweza tu kumfundisha mwenyewe nyumbani.)
Machozi yalimbubujika Thomas baada ya kugundua kumbe, mama yake hakumsomea ukweli wa kilichoandikwa kwenye barua miaka ile na kwa hisia kali, Thomas aliandika kwenye shajara (diary) yake maneno haya: (Thomas Alva alikuwa ni mtoto mgonjwa wa akili ambaye, mama yake alimbadili na uwa genius kwa kauli moja tu.)
FUNZO: Neno moja, kauli moja, barua moja au uongo mmoja, unaweza kumbadili mtu mara moja. Kila mmoja, atumie neno la faraja na matumaini kumbadili mtu aliyeshindikana au kukataliwa.
Credit @ Maundu Mwingizi (Mwanabalagha).