Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Pete Tanzania ‘CHANETA’ imeendesha mafunzo ya awali kwa walimu wa shule za Msingi na Sekondari wilayani humo.
Kozi hiyo maalum imelenga kuhamasisha walimu kujikita katika mchezo huo ambao ni kama ulikuwa umesahaulika wilayani Meatu, hivyo Uongozi umedhamiria kuurudisha kwa kasi kupitia shule za Msingi na Sekondari.
Kozi hiyo ya siku tisa ilihusisha washiriki 27, ambapo Wanawake walikuwa 17 na Wanaume 10 huku wote wakipata alama za juu, hali ambayo imetoa Nuru njema kwa mchezo wa Mpira wa Pete wilayani humo.
Akizungumza na Dar 24 Media baada ya kukamilisha mafunzo ya Kozi hiyo, Mkufunzi Mkuu wa Kozi hiyo kutoka CHANETA Shila Simon Mwanchese amesema, amefurahishwa na uelewa wa washiriki wote, na naamini ni mwanzo mzuri kwa Wilaya ya Simiyu kuwa na muamko mzuri wa mchezo wa Mpira wa Pete.
Amesema kozi hiyo iliyokuwa na hadhi ya kimkoa imefanyika wilayani humo kwa mara ya kwanza mwaka huu, na anatarajia kuona kozi kama hizo zikiendelea mara kwa mara.
“Kwa ujumla mafunzo yamekwenda vizuri sana na nimefurahishwa kuona washiriki wote kupata alama za juu, ninaamini huu ni mwanzo mzuri na matokeo yake yataanza kuonekana kupitia shule za msingi na sekondari za wilaya hii,”
“Tumekuwa pamoja katika elimu ya Nadharia na Vitendo na wakati wote washiriki walinipa ushirikiano wa kutosha, hadi tumemaliza kozi hii.” amesema Mwanchese.
Naye Afisa Michezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Hassan Sengule amesema, dhumuni kubwa la kufanyika kwa Kozi hiyo wilayani hapo ni kuongeza muamko wa mchezo wa Mpira wa Pete, baada ya kuona kuna idadi ndogo ya makocha na wachezaji wa mchezo huo.
Sengule amesema kupitia kozi hiyo anaamini washiriki wote ambao walitoka katika shule za Msingi na Sekondari watakuwa chachu ya kwenda kufundisha kupitia shule zao, ili kupata wachezaji wenye umri mdogo ambao watakuwa chachu kwa wilaya ya Meatu na taifa kwa ujumla siku za usoni.
“Kumekuwa na muamko mdogo sana hapa wilayani kwetu, hivyo tuliona kuna haja ya kuwa na Kozi hii ambayo ina lengo la kupeleka muamko katika shule zetu ambako ndipo kuna vijana ambao wanaweza kufundishwa na kuwa wachezaji wazuri siku za usoni.”
“Huu ni mwanzo, tukijaaliwa mwakani tutakuwa na kozi nyingine kama hii ili kuendelea kutoa chachu kwa walimu kutoka katika shule zetu, tunaamini washiriki wote wanakwenda kuanza kazi ya kutoa elimu kwa vitendo kwa vijana kwenye shule zetu.” amesema Sengule
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa CHANETA Mkoa wa SIMUYU Costancia Conerly Kisege amekiri kufurahishwa na hatua ya kujitokeza kwa wingi kwa washiriki katika kozi hiyo.
Amesema naamini mafunzo yaliyotolewa katika Kozi hiyo ya awali yataleta matokeo chanya ambayo yatafanikisha mkoa wa Simiyu kuwa na timu bora kwa siku za usoni.