Klabu ya Newcastle United imethibitisha kuwa kiungo Sandro Tonali anachunguzwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Italia na Shirikisho la Soka la Italia ‘FIGC’ kuhusiana na madai ya kujihusisha na kubeti.
Tonali mwenye umri wa miaka 23 hivi majuzi aliondolewa kwenye kambi ya mazoezi ya Italia kutokana na kukutwa na mashtaka ya kujihusisha na kamari.
Newcastle wanasema Tonali anashirikiana na mamlaka kwa uchunguzi huo: “Yeye na familia yake wataendelea kupokea uungwaji mkono kamili wa klabu. Kutokana na mchakato huu unaoendelea, Sandro na Newcastle United hawawezi kutoa maoni zaidi kwa sasa.”
Tonali na mchezaji vwa Aston Villa, Nicolo Zaniolo hivi majuzi waliondoka kwenye kambi ya Italia kwa ajili ya mechi za kufuzu Euro 2024 dhidi ya Malta na Uingereza baada ya kuambiwa walihusika katika uchunguzi wa waendesha mashtaka wa Italia.
Tonali, ambaye amecheza mechi 15 na Italia, alijiunga na Newcastle kutoka AC Milan mwezi Julai kwa uhamisho wa Pauni 55m.
Juzi Jumanne, kiungo wa Juventus Nicolo Fagioli alifungiwa kwa miezi saba na Shirikisho la Soka la Italia kwa kukiuka sheria za Kamari huku pia akipigwa faini ya euro 12,500.