Mshambuliaji Neymar da Silva Santos Júnior amesema amehamia ligi yenye ushindani mkubwa kwa kujiunga na Al Hilal ya Saudi Arabia na kumsifu, Cristiano Ronaldo kwa ushawishi licha ya kuitwa kichaa alipohamia Mashariki ya Kati hapo mwezi Desemba, mwaka jana.
Mshambuliaji huyo wa Brazil, Neymar, aliwaacha mabingwa wa Ufaransa Paris Saint-Germain na kujiunga na Al Hilal yenye makao yake Riyadh, mabingwa watetezi wa bara la Asia, kwa uhamisho wa thamani ya dola milioni 98.6.
Nyota huyo wa zamani wa Barcelona mwenye umri wa miaka 31 alikuwa akihusishwa na kuhamia Manchester United, Chelsea au kurejea Camp Nou msimu huu wa joto, lakini akaamua kujiunga na Al Hilal.
“Ninaamini Cristiano Ronaldo alianzisha haya yote na kila mtu alimwita ‘kichaa’, na hivi na vile,” amesema Neymar.
“Leo unaona ligi inakua zaidi na zaidi. Ligi itakuwa na ushindani mkubwa hasa baada ya usajili uliofanyika kwenye dirisha la usajili la majira ya joto, naamini ushindani ni muhimu ndiyo maana najiunga na ligi hii, ninasukumwa na changamnoto, nipo kusaidia ligi kukua.
“Nina furaha sana kuandika historia mpya ya kufuatilia malengo yote na klabu na wachezaji wenzangu, kushinda mataji zaidi na zaidi na kutimiza azma ya klabu.”
Neymar, ambaye anaripotiwa atakuwa akipokea mshahara wa kila mwaka wa dola milioni 10 katika klabu ya Al Hilal, anafanya idadi ya uhamisho kwenda Saudi Arabia kutoka Ligi Kuu za Ulaya (England, Ufaransa, Hispania, Italia, Ujerumani na Ureno) kufikia zaidi ya 30.