Mshambuliaji ghali duniani Neymar da Silva Santos Júnior usiku wa kuamkia leo aliifungia Paris St Germain mabao mawili kati ya mabao sita kwa mbili yaliyoipa ushindi klabu hiyo ya jijini Paris dhidi ya Toulouse.
Neymar aliyesajiliwa kwa Euro milioni 222 sawa na dola za kimarekani milioni 260.92, ameendelea kuchukua nafasi katika vyombo vya habari duniani baada ya kuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha PSG ambacho kimedhamiria kurejea kwenye mafanikio ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliifungia PSG bao la kusawazisha, baada ya Max Gradel kuifungia Toulouse bao la kuongoza dakika ya 18. Adrien Rabiot aliongeza bao la pili kabla ya Edinson Cavani hajafunga bao la tatu kwa mkwaju wa penati.
Bao la nne la PSG lilikwamishwa wavuni na Marco Verratti dakika ya 69, lakini Toulouse walionyesha hali ya kutaka kujipapatua kwa kupata bao la pili kupitia kwa Christopher Jullien, ila hali iliwaendea kombo kwa kufungwa bao la tano, safari hii likifungwa na Javier Pastore.
Neymar alimaliza kupigilia msumari wa mwisho kwa kufunga bao la sita na kukamilisha ushindi wa tatu mfululizo kwa PSG katika ligi ya nchini Ufaransa.
Ushindi huo unaiwezesha PSG kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ya nchini Ufaransa kwa kufikisha point 9, sawa na mabingwa watetezi AS Monaco ambao wanazidiwa kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.
Matokeo ya michezo mingine ya ligi ya Ufaransa iliyochezwa jana.
Lille 0 – 2 Caen
Olympic Marseille 1 – 1 Angers