Meneja wa klabu bingwa nchini Ufaransa Paris Saint-Germain Thomas Tuchel, amesema mshambuliaji Neymar da Silva Santos, yupo kwenye hati hati ya kuukosa mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya 16 bora wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Brazil hakua sehemu ya kikosi cha Paris Saint-Germain, kilichopambana na Dijon usiku wa kuamkia leo Al-Khamis, katika michuano ya kombe la Ufaransa (Coupe de France). Katika mchezo huo Dijon walikubali kichapo cha bakora sita kwa moja.
Neymar aliumia mbavu akiwa katika mchezo wa ligi ya Ufaransa dhidi ya Montpellier uliochezwa Februari Mosi, na kwa siku kadhaa amekua akifanyiwa matibabu ili kuirejesha afya yake.
“Siwezi kusema kama atakuwa Fit kwa asilimia 100, kwa ajili ya kucheza dhidi ya Borussia Dortmund.” Alisema Tuchel alipokua akijibu maswali kwenye mkutano na waandishi wa habari.
“Tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya hali yake, huenda siku ya ijumaa tukapata uhakika kama ataweza kuwa sehemu ya safari ya kuelekea Ujerumani. Lakini hatuwezi kumuweka katika hali ya hatari zaidi, kama atakua hajapona sawa sawa.”
“Pia hatutaweza kumtumia katika mchezo wetu wa ligi dhidi ya Amiens, hata kama atakua Fit kucheza, kwa sababu hatutaki kubahatisha na badala yake tukajiharibia kabisa, katika mipango ya kumtumia kwenye mchezo wetu wa jumanne dhidi ya Borussia Dortmund.”
Paris Saint-Germain wanatarajiwa kuanza safari ya Ujerumani kuifuata Borussia Dortmund, mara baada ya kukamilisha mchezo wao wa ligi ya Ufaransa mwishoni mwa juma hili dhidi ya Amiens.
Michezo mingine ya ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya 16 bora.
Liverpool vs Atletico Madrid
Real Madrid vs Manchester City
Chelsea vs Bayern Munich
Lyon vs Juventus
Barcelona vs Napoli
Tottenham vs RB Leipzig
Atalanta vs Valencia