Mshambuliaji kutoka nchini Brazil Neymar da Silva Santos Júnior, amesema hana mpango wa kuikacha klabu yake ya Paris Saint-Germain inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Ufaransa (Ligue 1) na kutimkia mahala pengine, kama inavyoripotiwa katika vyombo vya habari.
Neymar amekanusha taarifa hizo, na kusisitiza anahitaji kubaki na mabingwa hao wa Ufaransa kwa lengo la kusaka mafanikio yaliyokususdiwa na uongozi wa ngazi za juu wa klabu hiyo.
Mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid wanatajwa kuwa katika harakati za kumsajili mshambuliaji huyo, ambaye pia ni nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Brazil, ili kuziba pengo lililoachwa wazi na Cristiano Ronaldo aliyejiunga na Juventus ya Italia.
“Sina mahala pa kwenda, nitabaki PSG kwa lengo la kuisaidia klabu yangu, ninaheshimu hisia za wengine, sichukizwi wanavyoendelea kuzungumzia hatua za kuhama kwangu, lakini msisitizo wangu ni kubaki Ufaransa.” Alisema Neymar’.
“Sitobadilisha msimamo wangu, kwa sababu ninaamini PSG wanahitaji huduma yangu kwa minajili ya kutetea ubingwa wa Ufaransa msimu ujao na kufanya vizuri katika michuano ya Ulaya.”
Neymar alisajiliwa na PSG msimu wa 2017/18 akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona kwa ada ya Euro milioni 222, na mpaka sasa ameshawatumikia mabingwa hao wa Ufaransa katika michezo 20 ya ligi na kufunga mabao 19.