Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil Neymar da Silva Santos Júnior, ameahidi kulipa fadhila na kuacha kumbukumbu nzuri kwa mashabiki wa klabu yake ya Paris Saint-Germain, inayoshiriki ligi ya Ufaransa pamoja na ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu wa 2019/20.
Neymar ameahidi kufanya hivyo, kutokana na kusudio lake la kutaka kuihama Paris Saint-Germain kukwama dakika za mwisho kabla ya dirisha la usajili halijafungwa mwanzoni mwa mwezi huu, hivyo ameona kuendelea kubaki klabuni hapo, na kurejesha fadhila kwa mashabiki.
Juzi jumamosi mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, aliifungua Paris Saint-Germain bao pekee na la ushindi dhidi ya Strasbourg katika mchezo wa ligi ya Ufaransa (Ligue 1), huku akikabiliwa na changamoto ya kuzomewa na mashabiki ambao walimuona kama msaliti kwa kitendo chake cha kutaka kuondoka wakati wa majira ya kiangazi.
Neymar aliweka wazi kwamba alitaka kuachana na Paris Saint-Germain ili arudi zake FC Barcelona, lakini uhamisho huo ulishindwa kukamilika na hivyo ataendelea kuwepo klabuni hapo msimu huu, na amesisitiza kufanya kazi kadri awezavyo ili kuwaridhisha mashabiki, ambao kwa sasa wanamuona kama adui kwao.
“Sina ujumbe wowote maalumu kwa mashabiki wa PSG. Nimeshazoea kuzomewa karibu maisha yangu yote ya soka. Nafahamu, msimu huu nitacheza michezo yote kama vile nipo ugenini.
“Kila mtu anafahamu wazi nilitaka kuondoka. Nilisema na narudia kusema. Sitaki kusema sana, ukurasa umeshafungwa. Mimi ni mchezaji wa PSG na sasa nitajitolea kila kitu kilichopo ndani ya uwezo wangu huko uwanjani.”
Tayari kuna tetesi Neymar huenda akauzwa mwezi Januari wakati wa dirisha dogo la usajili, na klabu nguli za Hispania Real Madrid na FC Barcelona zinapewa nafasi kubwa ya kumsajili.