Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Brazil Neymar Jr, huenda akasubiri hadi Septemba ili kuanza kuichezea timu ya A-Hilal ya Saudi Arabia kutokana na maumivu, amesema kocha Jorge Jesus.
Neymar alijiunga na Al-Hilal akitokea klabu ya Paris St Germain (PSG) Jumanne iliyopita kwa mkataba wa miaka miwili, ambao gazeti la Ufaransa la L’Equipe lilisema kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 anapata kiasi cha Dola za Marekani milioni 174 (sawa na Sh bilioni 434).
“Neymar ni mchezaji mbunifu, atatusaidia kuimarika zaidi, lakini kwa sasa amepata majeraha madogo na sijui atarudi lini uwanjani. Labda atakuwa tayari katikati ya Septemba, “alisema Jesus baada ya hafla ya kumkabirisha mbele ya watazamaji 60 000 kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Mfalme Fahd juzi Jumamosi (Agosti 19).
Ndege za kupiga picha zisizo na rubani ziliruka juu ya uwanja wa nyumbani wa A-Hilal kutangaza kuwa “Neymar ní Bluu ” kabla nyota huyo wa zamani wa FC Barcelona hajashuhudia timu yake ikitoka sare ya 1-1 dhidi ya Al-Fayha.