Mshambuliaji wa Brazil, Neymar amesema hayuko sawa kabisa kucheza katika mechi mbili za kwanza za kufuzu fainali zijazo za Kombe la Dunia kutokana na jeraha la kifundo cha mguu wa kulia ambalo limemweka nje tangu Februari, mwaka huu Neymar aliondoka Paris Saint-Germain na kwenda Al-Hilal ya Saudi Arabia lakini bado hajaichezea klabu yake hiyo mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Neymar alisema Ligi Kuu ya Saudia inaweza kuwa bora kama Ligue l ya Ufaransa.
Jana Brazil ilicheza mechi yake ya kwanza katika safari ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 katika mji wa Amazon wa Belem dhidi ya Bolivia na wataondoka kuifuata Peru ambayo watavaana nayo hapo Jumanne.
Neymar alifafanua hali yake ya jeraha kabla ya mechi hizo baada ya Kocha wa Al-Hilal, Jorge Jesus, kulikosoa Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) kwa kumwita akiwa bado hana hali ya kucheza.
Mchezaji huyo wenye umri wa miaka 31, alisema amejiunga na Brazil katika hali kama hiyo hapo awali na bado alicheza.
“Ninajisilkia vizuri, mwenye furaha, lakini ni wazi siko fiti kwa asilimia 100%. Lakini kichwa changu kipo vizuri, mwili wangu uko vizuri,” alisema Neymar.
“Nilikuwa naenda kucheza mechi ya hivi karibuni zaidi ya Al Hilal, lakini kocha alichagua kuniacha nje, ili nije Brazil”
Mechi ya mwisho zaidi ya Neymar akiwa na Brazil ilikuwa ni kupoteza dhidi ya Croatia katika hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Dunia.
Aliondoka Qatar akiwa na shaka kuhusu mustakabali wake katika timu ya taifa na hakucheza mechi tatu za kwanza za Selecao mwaka huu.
“Baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa familia na marafiki kurejea kwenye timu ya taifa unaanza kutoa thamani kwa kila ulichofanya.” aliongeza Neymar.
“Unapokuwa na watu wako, familia yako, wanakuweka kwenye nafasi yako na kukufanya uone inafaa kuendelea kuwa na furaha kwa kuvaa jezi ya Brazil”
Neymar anahitaji bao moja ili kuipiku rekodi ya mabao 77 ya Pele kama mfungaji bora wa Brazil kwa wakati wote.