Katika kuhakikisha kuwa mazao yaliyovunwa katika msimu wa mwaka 2022/2023 yanapata soko la uhakika, bei nzuri na nchi kuwa na uhakika wa usalama wa chakula, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula – NFRA, imepanga kununua tani 305,000 za Nafaka.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa kuahirisha Mkutano Wa 12 wa Bunge jijini Dodoma na kuongeza kuwa hadi kufikia Septemba 5, 2023, jumla ya tani 175,000 za nafaka sawa na asilimia 57 za lengo zimeshanunuliwa kupitia katika vituo 75 vilivyopo katika kanda nane za NFRA.
Amesema, “nitumie fursa hii kuielekeza Wizara ya Kilimo kupitia NFRA kuimarisha miundombinu ya uhifadhi ili kuepuka kupoteza mazao ya chakula wanayoendelea kununua. katika msimu 2022/2023 bei za mazao mengine ya biashara
zimeendelea kuimarika hususan mazao yanayotumia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani.”
Majaliwa amebainisha kuwa, zao la kakao linalolimwa kwa wingi Wilaya za Kyela na Mvomero bei imefikia shilingi 8,700 kwa kilo huku Mbaazi bei imeongezeka kutoka shilingi 1,000 – 1,500 kwa kilo hadi shilingi 2,000 kwa Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi na shilingi 2,200 kwa Mkoa wa Manyara.